WANAFUNZI WA SHULE YA SEKONDARI MAHIWA WAJITOKEZA KWA WINGI KUCHANGIA DAMU.

Katika kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha upatikanaji wa damu salama kwa ajili ya kuokoa maisha ya wagonjwa, timu ya huduma ya uchangiaji wa damu kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mt.Walburga Nyangao Julai,25,2026 imetembelea Shule ya Sekondari Mahiwa kwa lengo la kutoa elimu na kuhamasisha wanafunzi kushiriki katika uchangiaji wa damu kwa hiari.Wakizungumza wakati wa zoezi hilo, wataalamu kutoka hospitali ya rufaa ya Mt. Walburga Nyangao walieleza kuwa damu ni rasilimali muhimu ambayo haiwezi kutengenezwa viwandani, hivyo inapatikana kupitia watu wanaojitolea kuchangia.

Aidha walihimiza wanafunzi wenye sifa za kuchangia damu kufanya hivyo kwa hiyari ili kusaidia kuokoa maisha ya akina mama wajawazito, watoto, waathirika wa ajali na wagonjwa wengine wanaohitaji huduma hiyo.

Katika elimu iliyotolewa, wanafunzi walifafanuliwa kuhusu umuhimu wa uchangiaji wa damu, vigezo vya kuwa mchangiaji salama, pamoja na kuondoa dhana potofu zinazoweza kuwazuia watu kushiriki katika zoezi hilo.

Wanafunzi walipata fursa ya kuuliza maswali mbalimbali yaliyopatiwa majibu na wataalamu wa afya.Kwa upande wao Uongozi wa Shule ya Sekondari Mahiwa uliishukuru Hospitali ya Rufaa ya Mt. Walburga Nyangao kwa kufikisha elimu hiyo muhimu, ukieleza kuwa imeongeza uelewa wa wanafunzi kuhusu wajibu wao katika kuokoa maisha ya wengine kupitia uchangiaji wa damu kwa hiari.

Hospitali ya Rufaa ya Mt. Walburga Nyangao inaendelea kuhimiza jamii kujitokeza kuchangia damu mara kwa mara, kwani kila tone la damu linaweza kuwa tumaini la uhai kwa mgonjwa anayehitaji huduma hiyo.