WAKUU WA IDARA MT. WALBURGA WAKETI KUJADILI UTEKELEZAJI WA SHUGHULI MBALIMBALI.
Wakuu wa idara wa Hospitali ya Rufaa ya Mt. Walburga Nyangao, Julai 30, 2026, walikutana katika ukumbi wa mikutano wa hospitali hiyo kwa ajili ya Kikao cha Timu ya Menejimenti ya Hospitali (HMT), kilicholenga kujadili utekelezaji wa shughuli mbalimbali pamoja na kupanga mikakati ya kuendelea kuboresha huduma za afya zinazotolewa kwa wananchi.
Kikao hicho kilijadili ajenda mbalimbali muhimu, ikiwemo taarifa ya fedha, mapato na matumizi kwa kipindi cha miezi sita kuanzia Januari hadi Juni 2026. Wajumbe walipitia mwenendo wa makusanyo ya mapato, matumizi yaliyofanyika pamoja na kujadili mikakati ya kuimarisha usimamizi wa rasilimali fedha ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.
Aidha, kikao kilipokea na kujadili maendeleo ya Master Plan ya ujenzi wa jengo la Maternity Complex, mradi unaotarajiwa kuongeza uwezo wa hospitali katika kutoa huduma bora za afya ya mama na mtoto. Vilevile, wajumbe walijadili maendeleo ya ujenzi wa jengo la Pharmacy, ambalo linatarajiwa kuboresha upatikanaji, uhifadhi na usimamizi wa dawa na vifaa tiba.
Kwa ujumla, kikao hicho kilisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya idara zote katika kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa, sambamba na kuendelea kuimarisha uwajibikaji, matumizi sahihi ya rasilimali na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.


